Ali Mohammadi, naibu afisa wa masuala ya kisiasa katika Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi (IRGC), akirejelea kauli za Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu kudhibiti wa Lango la Hormuz, alisema: "Ikiwa ndivyo ilivyo, kwa jina la Mungu, leteni mojawapo ya meli zenu ndani ya umbali wa kilomita 100."
Muhtasari
Urusi na Ukraine zashambuliana vikali
Watu 1,400 watoroka Yemen na kuingia Djibouti ndani ya saa 24 pekee - Waziri wa Fedha wa Djibouti
Vikosi vya Urusi vilirusha ndege zisizo na rubani almaarufu droni 453 kuelekea Ukraine usiku wa Jumapili, kulingana na ripoti ya Jeshi la Anga la Ukraine.
Kwa mujibu wa Jeshi la Ukraine, mashambulizi yaliripotiwa katika maeneo 13, huku mabaki ya vifaa hivyo yakianguka katika maeneo mengine 7.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mkoa wa Donetsk iliripoti kupitia chaneli yake ya Telegram kwamba raia wawili waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa katika shambulio la Urusi lililofanywa asubuhi dhidi ya mji wa Kramatorsk.
Shambulio hilo lilitokea saa nne asubuhi na kulenga gari la abiria. Vikosi vya Urusi vilidondosha mabomu manne ya angani ya aina ya FAB-250 katika mji huo. Kwa sasa, watu sita wanaripotiwa kujeruhiwa.
Watu 1,400 watoroka Yemen na kuingia Djibouti ndani ya saa 24 pekee - Waziri wa Fedha wa Djibouti
Waasi wa
Houthi sasa wako umbali wa kilomita 20 tu kutoka Djibouti baada ya kuteka mji
wa bandari wa Mocha, jambo linalowaweka karibu zaidi na Mlango-bahari wa
kimkakati wa Bab al-Mandeb, njia muhimu ya usafirishaji wa meli duniani
inayounganisha Bahari ya Shamu na Mfereji wa Suez.
Katika
ujumbe kwenye mtandao wa X, Waziri Ilyas Moussa Dawaleh alisema kuwa wakimbizi
1,400 walikuwa wamewasili kutoka Yemen ndani ya saa 24.
Siku moja
kabla, alisema takriban watu 500, wakiwemo wanawake na watoto, walikuwa
wamefika katika mji wa pwani wa Obock baada ya kuokolewa baharini wakati boti
zao zilipokwisha mafuta walipokuwa wakivuka mlango-bahari huo.
Mji huo wa
Obock, ulio umbali wa zaidi ya kilomita 20 kutoka Yemen, kwa muda mrefu umekuwa
eneo muhimu la kuwasili kwa watu wanaokimbia nchi hiyo iliyoathiriwa na vita.
Waasi wa
Houthi waliteka mji wa bandari wa Mocha katika Bahari ya Shamu na eneo la pwani
siku ya Alhamisi, na kuwalazimu maelfu ya familia kukimbia.
Mlango-bahari
mwembamba wa Bab-el-Mandeb pia hutumiwa kama njia ya uhamiaji na wahamiaji
kutoka Pembe ya Afrika wanaovuka kuingia Yemen wakijaribu kufika nchi za Ghuba.
Wimbi hili
la hivi karibuni la kuwasili kwa watu linakuja wakati idadi ya watu waliokimbia
makazi yao ndani ya Yemen ikiongezeka. Shirika la Kimataifa la Uhamiaji
linasema makumi ya maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao kutokana na mapigano
mapya yaliyoanza mwezi Julai.
6 wafariki, 107 waokolewa kwenya ajali ya kivuko huko Java, Indonesia
Watu sita
wamefariki dunia huku wengine 107 wakiokolewa kutoka kwenye chombo cha majini
{Ferry/kivuko} cha abiria cha Indonesia kilichokumbwa na matatizo katika Bahari
ya Java, kulingana na shirika la Indonesia la utafutaji na uokoaji.
Operesheni
ya utafutaji na uokoaji ilianzishwa baada ya mawasiliano kupotea na meli ya
{Virgo Transport 8}, iliyokuwa na watu 243, wakati ilipokumbana na hali mbaya
ya hewa, shirika hilo lilisema.
Shughuli za
kuwatafuta abiria waliosalia
zinaendelea.
Kivuko hicho
kilikuwa kikisafiri kutoka Surabaya kuelekea mji wa Banjarmasin katika eneo la
Kalimantan Kusini, na taarifa za mwisho zilionyesha kuwa kilikuwa umbali wa
takriban kilomita 150 (maili 93) kusini mwa Banjarmasin majira ya saa 02:00
asubuhi kwa saa za eneo hilo siku ya Jumapili (saa 18:00 GMT siku ya Jumamosi).
Mamlaka
zilipokea taarifa ya awali ya dharura saa 04:10 kutoka kwa kampuni inayoendesha
meli hiyo, PT Virgo. Meli hiyo iliondoka Surabaya saa 10:33 siku ya Jumamosi na
ilitarajiwa kuwasili Banjarmasin siku ya Jumapili saa 14:00, kulingana na
taarifa kutoka tovuti mbili zinazofuatilia usafiri wa baharini.
Kikosi kazi
cha pamoja kinachohusisha shirika la Indonesia la utafutaji na uokoaji, jeshi
la wanamaji, polisi wa majini na wadau wengine kimeundwa kwa ajili ya shughuli
hiyo ya uokoaji.
Meli na
helikopta zimetumwa eneo la tukio, huku wafanyakazi 280 wakishiriki katika
operesheni hiyo ya uokoaji. Meli zote zilizopo katika eneo la Bahari ya Java
zimearifiwa kuripoti dalili zozote za kuwepo kwa abiria.
Kituo cha
uendeshaji kwa ajili ya kushughulikia ajali hiyo kilianzishwa katika eneo la
Bandari ya Trisakti siku ya Jumapili asubuhi.
Kuna abiria
213 na wafanyakazi 30 wa meli hiyo. Kati yao, watu 130 bado hawajulikani
walipo.
Rusmilawati,
mkazi wa Banjarmasin, alienda bandarini kutafuta taarifa kuhusu ndugu zake
wanane waliokuwa abiria kwenye meli hiyo. Walikuwa wakirejea Banjarmasin baada
ya kutembelea makaburi ya wanazuoni kadhaa wa Kiislamu huko Java.
"Awali
walisafiri kwa ndege kwenda huko, lakini kwa safari ya kurudi walitaka kujaribu
kusafiri kwa meli," aliambia BBC Indonesia.
Kufikia
alasiri ya Jumapili kwa saa za huko, Rusmilawati alisema hakuwa amepata taarifa
yoyote kutoka kwa maafisa kuhusu iwapo ndugu zake walikuwa wameokolewa.
Senegal ipo tayari kwa michezo ya Olimpiki ya vijana 2026
Mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya Vijana umewasili nchini Senegal kwa ajili ya safari ya kuuzungusha nchi nzima.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa taifa hilo la Afrika Magharibi kuwa mwenyeji wa mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika katika ardhi ya Afrika.
Mwenge huo ulipokelewa katika mji mkuu wa Senegal baada ya kuwashwa katika Uwanja wa kihistoria wa Panathenaic jijini Athens, Ugiriki, Alhamisi iliyopita.
Michezo ya Olimpiki ya Vijana itafanyika kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi 13 Novemba katika maeneo ya Dakar, Diamniadio na Saly, huku takriban wanariadha 2,700 wakitarajiwa kushiriki katika michezo 25 tofauti.
Tukio hili litakuwa hatua muhimu ya kihistoria kwa Senegal na bara zima, huku sherehe zikiwakutanisha vijana, wanariadha, wadau wa utamaduni, na viongozi wa jamii katika hafla ya kuhesabu siku zilizosalia iliyofanyika Dakar siku ya Jumamosi.
Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), Kirsty Coventry kutoka Zimbabwe, alihudhuria hafla hiyo katika eneo la Place du Souvenir jijini Dakar, ambapo mwenge huo uliwashwa.
Coventry, ambaye ni Mwafrika wa kwanza na mwanamke wa kwanza kuongoza IOC, alielezea Michezo hiyo kama fursa ya kuleta athari ya kudumu kwa vijana kote barani.
"Lengo ni kwamba haitaleta athari kwa vijana wanaokuja hapa pekee, bali wanaporejea nyumbani, watazungumzia maadili na hamasa iliyotokana na Michezo hiyo ndani yao," alisema Coventry.
Aliongeza kuwa safari ya mwenge huo nchini Senegal itasaidia kuongeza uelewa kuhusu tukio hilo muhimu na kuhamasisha jamii kote nchini.
Mwenge huo utapita katika mikoa 14 ya Senegal kama sehemu ya ziara iliyolenga kuleta roho ya Michezo hiyo karibu na jamii za wenyeji kabla ya kurejea Dakar kwa ajili ya sherehe ya ufunguzi mwezi ujao.
Michezo ya Dakar 2026 imesifiwa sana kama wakati muhimu kwa michezo barani Afrika, ikitoa jukwaa lisilo na kifani la kuonyesha vipaji vya vijana, utamaduni, na uwezo wa kuandaa matukio makubwa barani humo.
Waandaaji wanatumai kuwa Michezo hiyo itaacha alama katika nyanja za maendeleo ya vijana, elimu, na ushiriki katika michezo, huku ikiimarisha nafasi inayokua ya Afrika katika harakati za kimataifa za Olimpiki.
Akili unde yatishia maisha ya binadamu, wasema wataalamu
Mtafiti wa akili bandia (AI) aliyeacha kazi katika kampuni ya Anthropic amesema kuwa watu wanaoshughulikia teknolojia hiyo walikuwa na "hofu" kuhusu kasi ya maendeleo yake na nini inaweza kumaanisha kwa wanadamu.
Jacob Coxon alimweleza mwandishi wa BBC Laura Kuenssberg katika mahojiano kuhusu ujumbe wake wa kujiuzulu uliosambaa sana, ambapo alielezea wasiwasi wake kuhusu AI inayokwenda bila udhibiti.
"Ninaamini kwamba tusipopunguza kasi ya maendeleo ya sasa, kuna uwezekano mkubwa kwamba sote tunaweza kupoteza maisha katika siku za usoni," alisema.
Hatua yake ya kujiuzulu inakuja wakati kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu usalama katika sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na maoni kutoka kwa bosi wake wa zamani, mkuu wa Anthropic Dario Amodei, ambaye katika makala alitetea wazo la kupunguza kasi ya maendeleo.
Viongozi wa kampuni mbili pinzani za AI, Sam Altman wa OpenAI na Elon Musk wa xAI, wote wamesema wanaunga mkono pendekezo la Amodei la kupunguza kasi na kuweka udhibiti katika sekta nzima, pamoja na ufuatiliaji huru wa uundaji wa mifumo ya AI.
Amodei alisema kuwa suala la kuendeleza teknolojia hiyo halina shaka, lakini hatari zinazohusiana nayo ni "kubwa", na kwamba makampuni pamoja na serikali lazima vipewe muda wa kushughulikia changamoto hizo.
Coxon, mwenye umri wa miaka 27—ambaye aliwahi kufanya kazi OpenAI kabla ya kujiunga na Anthropic—aliunga mkono wazo la kupunguza kasi lakini akasema hatua hiyo inahitaji kuratibiwa na China ili kuepuka "mashindano ya kimataifa".
Kulingana na Coxon, swali gumu zaidi kujibu lilikuwa ni jinsi maangamizi yanayosababishwa na Akili Bandia (AI) yangeonekana.
Moja ya hatari zilizotajwa katika maoni ya Amodei ilikuwa ni uwezekano wa kundi la programu-roboti (bots) kufanya kazi kama kompyuta kuu yenye nguvu (supercomputer) na kuweza kutawala mtandao.
Coxon alisema hali hii inaweza kuwa halisi ndani ya kipindi cha miezi sita hadi mwaka mmoja.
Kufuatia kuondoka kwa Coxon, msemaji wa kampuni ya Anthropic aliambia BBC News: "Siku zote tumekuwa wazi kwamba AI italeta faida kubwa na pia hatari ambazo hazijawahi kushuhudiwa.
Wadau wa sekta hiyo wamependekeza kuwa maoni kuhusu hatari na nguvu ya AI huenda yanalenga tu kuzua gumzo au taharuki. Wakosoaji wengine wanasema Anthropic imekuwa ikijaribu kuchochea hatua za udhibiti ili kuzuia ushindani, na hivyo kuiacha yenyewe na OpenAI zikitawala soko pekee (duopoly).
Inaripotiwa kuwa Anthropic inajiandaa kwa hatua ya kuuza hisa zake kwa umma kwa mara ya kwanza (IPO), hatua ambayo inaweza kuweka rekodi mpya.
OpenAI ilitarajiwa kufanya vivyo hivyo, lakini Altman alisema kuwa huo ungekuwa "wakati usiofaa" kufanya hivyo "kutokana na hali ya sasa kuhusu masuala ya usalama," katika mahojiano na jarida la Fortune siku ya Ijumaa.
Hata hivyo, Coxon alikuwa na matumaini fulani kuhusu mustakabali wa AI, akiambia BBC kuwa watu wanaofanya utafiti wa teknolojia hiyo "kwa dhati wanataka kuona matokeo chanya" ya mambo kama vile "kutatua matatizo ya magonjwa na kuboresha maisha ya kila mtu".
Kauli zake kuhusu AI zimesambazwa mara mamilioni kwenye mitandao ya kijamii, huku mwanasayansi wa Anthropic, Evan Hubinger, akijibu kwenye mtandao wa X kwamba anakubaliana na Coxon.
"Kwa kweli tunaamini kabisa kuwa AI inaweza kuua wanadamu wote! Binafsi nadhani kuna uwezekano wa zaidi ya asilimia 10 (10%) ndani ya muongo ujao," alisema Hubinger.
Watu mashuhuri katika nyanja ya AI wamekuwa wakitoa tahadhari kuhusu tishio la kiusalama linaloletwa na teknolojia hiyo kwa miaka mingi sasa, huku viongozi wa OpenAI, Google DeepMind, na Anthropic wakieleza hayo mwaka wa 2023.
Tahadhari hizi zimezidi kusikika kwa nguvu katika wiki za hivi karibuni, kadiri mifumo mipya inavyoonyesha uwezo mkubwa zaidi ambao huenda wabunifu wake wanapata changamoto kuudhibiti.
Mwezi Aprili, Anthropic ilisema kuwa inazuia mfumo wake wa 'Mythos' kutumiwa na umma kwa sababu unaweza kujiondoa wenyewe kutoka kwenye mazingira ya majaribio, yanayojulikana kama 'sandbox'.
OpenAI pia imesema kuwa baadhi ya hatua katika uundaji wa mfumo wake wa hivi karibuni wa 'Astra' zimesitishwa, ikitaja wasiwasi kuhusu usalama wa mtandaoni.
Uganda yaamrisha wanafunzi kutoka DRC kuwekwa karantini kwa siku 21 kabla ya kurejea shuleni
Serikali ya
Uganda imeamuru wanafunzi wanaosafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) kukaa karantini kwa lazima kwa siku 21 wakati muhula mpya wa masomo
ukianza.
Wanafunzi
wanaowasili kutoka DRC lazima wakamilishe kipindi cha siku 21 cha karantini,
muda ambao unaendana na kipindi cha maambukizi ya virusi vya Ebola kabla ya
dalili kujitokeza.
Katibu wa
Kudumu katika Wizara ya Elimu, Dkt. Kedrace Turyagyenda, amesema agizo hilo
limetolewa kufuatia tathmini ya kitaalamu ya hatari na kubainisha kuwa
wanafunzi hao waliowekwa karantini watafuatiliwa kwa karibu kabla ya kuripoti
katika shule zao husika.
Agizo hilo
limetolewa wakati shule zikijiandaa kufunguliwa kwa ajili ya muhula wa tatu.
Hatua hiyo
ni sehemu ya itifaki na tahadhari za kiafya zinazoendelea kutekelezwa katika
eneo hilo kufuatia milipuko ya Ebola katika baadhi ya maeneo ya DRC.
Uganda
ilitangazwa kuwa haina maambukizi ya Ebola mnamo tarehe 26 Agosti 2026, baada
ya kukamilisha kipindi cha lazima cha ufuatiliaji cha siku 42 kufuatia mgonjwa
wa mwisho kuruhusiwa kutoka hospitalini mnamo tarehe 16 Julai 2026.
Wakati huo
huo nchini DRC, mlipuko wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo
umeenea hadi eneo jipya la huduma za afya, na kufanya idadi ya walioathirika
kufikia 61 katika mikoa sita kati ya mikoa 26 ya nchi hiyo, Shirika la Afya
Duniani (WHO) limesema Alhamisi.
Katika
taarifa yake ya hivi karibuni, WHO ilisema mlipuko huo umeenea hadi eneo la
huduma za afya la Kayna katika mkoa wa Kivu Kaskazini tangu taarifa yake ya
tarehe 28 Agosti.
Kufikia
Septemba 7, nchi hiyo ilikuwa imeripoti visa 6,757 vilivyothibitishwa, ikiwa ni
pamoja na vifo 3,267, na kusababisha uwiano wa vifo vya wagonjwa wa 48.3%.
Mlipuko huo
unaathiri maeneo ya afya katika majimbo ya Bas-Uele, Haut-Uele, Ituri, Kivu
Kaskazini, Kivu Kusini na Tshopo.
WHO ilisema
mienendo ya maambukizi inabaki kuwa tofauti katika maeneo yaliyoathiriwa, huku
kukiwa na ushahidi wa upanuzi unaoendelea wa kijiografia na ongezeko endelevu
la visa katika baadhi ya maeneo ya afya.
Serikali ya
Kenya imeongeza juhudi za kudhibiti mlipuko wa Homa ya Nguruwe ambayoimeua karibu nguruwe 1,500 katika mashamba zaidi ya 20 katika Kaunti ya
Kiambu tangu Mei.
Idara ya
Huduma za Mifugo inasema ugonjwa huo pia umeripotiwa katika kaunti zingine
sita: Tharaka-Nithi, Embu, Kakamega, Busia, Homa Bay, na Migori ambapo visa na
vifo zaidi vimerekodiwa.
Mlipuko huo
umesababisha ufuatiliaji ulioimarishwa na hatua za kuzuia kuenea zaidi katika
mipaka ikiwa ni pamoja na kuzuia uhamaji wa mifugo.
Takriban
nguruwe 1,470 hadi 1,500 wamekufa Kiambu pekee, na kuwaathiri wakulima wa eneo
hilo vikali na kutishia maisha.
Mamlaka inasisitiza
kwamba Homa ya Nguruwe ya Afrika ni ugonjwa unaoambukiza unaoathiri nguruwe wa
kufugwa na wa porini, lakini hauambukizi binadamu.
Idara ya
Huduma za Mifugo (DVS) imeongeza ufuatiliaji, na udhibiti wa uhamaji wa mifugo kote nchini.
Serikali za
kaunti na mamlaka za kilimo zimepuuzilia mbalia taarifa ambazo zimezitaja kama
uvumi unaodai kwamba Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo la Kenya (KALRO)
lilisambaza watoto wa nguruwe walioambukizwa.
Tetesi: Arsenal kushindana na Real Madrid katika kumsajili Nico Paz
Arsenal
inamfuatilia Nico Paz, Liverpool na Aston Villa zinamtazama Cher Ndour, na
Sunderland haitaki kukata tamaa katika juhudi za kumsajili Geny Catamo.
Arsenal
inafuatilia maendeleo ya mshambuliaji wa Argentina anayechezea Como, Nico Paz
(22), lakini Real Madrid ina haki ya kumnunua tena kwa euro milioni 80 (pauni
milioni 68.7). (ElDesmarque – In Spanish)
Liverpool na
Aston Villa ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kiungo wa kati wa Italia
anayechezea Fiorentina, Cher Ndour (22). (Caught Offside)
Sunderland
haitaki kukata tamaa katika juhudi za kumsajili Geny Catamo kutoka Sporting
baada ya kushindwa kumnunua winga huyo wa Msumbiji (25) wakati wa dirisha la
usajili la majira ya joto. (Record, via Sport Witness)
Monaco
inaamini inaweza kupata euro milioni 70 (pauni milioni 60.1) kwa ajili ya
Lamine Camara kiungo wa kati wa Senegal mwenye umri wa miaka 22 anayewaniwa na
Chelsea na Liverpool ambaye uhamisho wake kwenda Stamford Bridge ulikwama
katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili. (TeamTalk)
Mshambuliaji
wa Ujerumani, Lukas Nmecha (25), anatarajia kuondoka Leeds United mkataba wake
utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu iwapo hatapata muda wa kutosha kucheza.
(Football Insider)
Celtic
inamfuatilia beki wa kushoto wa England anayechezea Liverpool, Luke Chambers (22),
huku ikitathmini uwezekano wa kumsajili katika dirisha la usajili la mwezi
Januari. (Football Insider)
Winga wa
Ivory Coast, Wilfried Zaha (33), amependekezwa kwa klabu ya Malaga baada ya
kuondoka Galatasaray kama mchezaji huru kufuatia vipindi viwili vya mkopo
katika timu ya MLS, Charlotte FC. (Mundo Deportivo – In Spanish)
Raphinha ana
mkataba na Barcelona hadi mwaka 2028, lakini mabingwa hao wa Uhispania tayari
wanatafakari kumpa winga huyo wa Brazil (29) nyongeza ya mkataba hadi mwaka
2030. (AS – In Spanish)
Pia, Barca
imekamilisha makubaliano ya kuongeza mkataba wa mshambuliaji wa Misri mwenye
umri wa miaka 18, Hamza Abdelkarim, hadi mwaka 2030, ikiwa na kipengele cha bei
ya kuvunja mkataba cha euro milioni 150 (pauni milioni 128.7). (Sport – In Spanish)
Arsenal na
Chelsea zinaongoza katika mbio za kumsajili winga wa Norway mwenye umri wa
miaka 15 anayechezea Valerenga, Gabriel Rajkovic. (TeamTalk)
Vuguvugu la kisiasa nchini Kenya Linda mwanachi lazuru Nairobi
Seneta wa
Nairobi Edwin Sifuna anakabiliwa na kibarua kigumu cha kisiasa Jumapili hii
anapojiandaa kupima umaarufu wake katika kaunti anayoiwakilisha katika Bunge la
Seneti la Nairobi kwa kuandaa mkutano mkubwa wa kisiasa.
Muungano wa
kiaissa wa Linda Mwananchi unapeleka kampeni yake mjini Nairobi katika ziara
kuu ya uhamasishaji inayotarajiwa kuhitimishwa kwa mkutano mkubwa katika Uwanja
wa Jacaranda ambao ulikuwa maarufu na mojawapo ya ngome za kisasa za kinara wa
zamani wa ODM Raila Odinga.
Ziara hiyo
ya Nairobi inayosubiriwa kwa hamu imeanza katika Kanisa Kuu la All Saints
ambapo kundi hilo lilifika saa tatu asubuhi kuhudhuria ibada ya Jumapili, kabla
ya vuguvugu hilo kuanza ziara katika baadhi ya masoko na maeneo yenye shughuli
nyingi jijini.
Polisi
wameshika doria katika maeneo mbalimbali Jijini Nairobi hasa Katikati mwa Jiji na kwenye barabara kuu
za Outering na Jogoo na vile vile katika uwanja huo wa Jacaranda.
Kutoka
kanisani, Sifuna na wafuasi wake wanatarajiwa kuelekea masoko ya Marikiti na
Gikomba kabla ya kuendelea hadi Soko la Burma.
Ratiba hiyo
kisha italipeleka vuguvugu hilo katika maeneo ya Stage 17, B Centre na
Manyanja, ikifuatiwa na maandamano kando ya Barabara ya Jogoo.
Ziara hiyo
imepangwa kuhitimishwa katika Uwanja wa Jacaranda mwendo wa saa nane mchana,
ambapo Sifuna anatarajiwa kuhutubia mkutano mkubwa.
Harakati
hizi za uhamasishaji jijini Nairobi zinafanyika wakati seneta huyo akijaribu
kupanua wigo wa Linda vuguvugu la Mwananchi nje ya msingi wake wa uungwaji
mkono unaokua, na kuonyesha kuwa vuguvugu hilo linaweza kuvutia wafuasi wengi
wa kisiasa jijini.
Sifuna
amewahimiza wafuasi wake kujitokeza kwa wingi katika tukio ambalo washirika
wake tayari wamelielezea kama "mama wa mikutano yote" .
Katika
ujumbe ulioshirikiwa kwenye mitandao ya kijamii, Sifuna aliwasilisha ratiba ya
Jumapili kama mchanganyiko wa maombi na uhamasishaji wa kisiasa, akiwataka
wafuasi kutokuwa na visingizio vya kutohudhuria.
Wahouthi watangaza mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi ya kijeshi ya Saudia
Kundi la
Houthi la Yemen limetangaza kuwa limeishambulia kambi ya kijeshi kusini mwa
Saudi Arabia kwa kutumia makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani.
Yahya Saree,
msemaji wa kijeshi wa kundi la Houthi, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X
kwamba shambulio hilo lililenga kambi ya Sharura iliyoko kusini mwa Saudi
Arabia.
Kwa mujibu
wake, mashambulizi hayo yalilenga "ghala za silaha pamoja na vituo vya
amri na udhibiti" vya Saudi Arabia.
Bw. Saree
hakutaja muda kamili wa shambulio hilo, lakini alionya kuwa kuendelea kwa hatua
za kijeshi dhidi ya Yemen kungesababisha mashambulizi makali zaidi na mapana
yatakayofika ndani kabisa ya ardhi ya Saudi Arabia.
IRGC yaonya dhidi ya meli za Marekani zinazokaribia mlango wa Hormuz
Ali
Mohammadi, naibu afisa wa masuala ya kisiasa katika Jeshi la Wanamaji la
Walinzi wa Mapinduzi (IRGC), akirejelea kauli za Rais wa Marekani Donald Trump
kuhusu kudhibiti wa Lango la Hormuz, alisema: "Ikiwa ndivyo ilivyo, kwa
jina la Mungu, leteni mojawapo ya meli zenu ndani ya umbali wa kilomita
100."
Afisa huyo
mwandamizi wa IRGC alisema: "Wamarekani wanajua kuwa iwapo meli zao
zitakaribia, zitakabiliwa na jibu kutoka kwa vikosi vya Iran," na bila
kutoa maelezo zaidi, alidai kuwa "mfano wa tukio kama hilo umeshuhudiwa
pia katika siku za hivi karibuni."
Akizungumza
katika mkutano wa usiku wa wafuasi wa serikali mjini Mashhad, alisema:
"Leo... hakuna wanajeshi wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi, Bahari ya
Oman, na Lango la Hormuz, wala hakuna vifaa vya Marekani vilivyowekwa katika
maeneo hayo. Iwapo Wamarekani watakaribia eneo hilo lililozuiliwa, wao wenyewe
wanajua nini kitawapata."
Kulingana
na yeye, "Meli yoyote inayotoka Kuwait na Bahrain, bila ubaguzi, huwa chini
ya uangalizi wa Jeshi la Wanamaji la IRGC, na iwapo ukiukwaji wowote
utabainika, hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa."
