Moja kwa moja, Trump aongeza muda wa kusitisha mashambulizi kwa siku 10 na kusema 'mazungumzo yanaendelea'
Rais wa Marekani amekuwa akisema kwa siku kadhaa kwamba mazungumzo kati ya Marekani na Iran yanaendelea, lakini Iran imekanusha kuendelea kwa hatua hiyo.
Muhtasari
Mashambulizi yafanyika usiku kucha kote Mashariki ya Kati
Marekani inajiandaa kwa 'shambulizi kubwa la mwisho' katika vita vya Iran
Watu 1,900 wameuawa nchini Iran tangu kuanza kwa vita
Afisa wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu alisema Ijumaa kuwa, kwa kuzingatia takwimu zilizotolewa na Hilali Nyekundu ya Iran, zaidi ya watu 1,900 wameuawa na takriban 20,000 wamejeruhiwa nchini Iran tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel.
Kwa mujibu wa BBC Arabic, Maria Martinez anasema kuwa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran ndilo shirika pekee la misaada la kitaifa ambalo linaendelea kufanya kazi kote nchini huku kukiwa na mzozo unaoongezeka.
Austria yapiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto chini ya miaka 14
Austria imekuwa nchi ya hivi karibuni katika Umoja wa Ulaya kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya miaka 14.
Hatua hiyo ilikuja baada ya mazungumzo ya muda mrefu ndani ya muungano wa serikali tawala.
Naibu kiongozi wa nchi hiyo, Andreas Babler, alisema ni vigumu kwa wazazi kuwalea watoto wao katika jamii hii, ambayo alisema imeundwa kwa makusudi kuwafanya wawe tegemezi.
Kiongozi wa upinzani Israel atoa wito Wayahudi wa dhehebu la Orthodox wasajiliwe jeshini
Nchini Israel, kiongozi wa upinzani Yair Lapid ameishutumu serikali kwa kuwatuma wanajeshi wachache sana vitani bila kuwepo kwa mkakati wowote.
Katika taarifa yake ya video kwa lugha ya Kiebrania, Yair Lapid alidai kuwa “jeshi la Israel limefikia uwezo wake wa juu kabisa na serikali inaacha wanajeshi wakimwaga damu katika uwanja wa vita.”
Aliongeza kuwa serikali “inatuma wanajeshi wachache sana katika vita vikubwa bila mkakati na bila rasilimali za kutosha. Wanajeshi wa akiba wamechoka na hawawezi tena kukabiliana na changamoto za kiusalama.”
Yair Lapid alitoa wito kwa serikali pia kuwaandikisha jeshini Wayahudi wa dhehebu la Ultra-Orthodox (Haredi). Kundi hili la Wayahudi linajulikana kuwa la kidini zaidi na limekuwa likisamehewa kufanya huduma ya lazima ya kijeshi tangu mwaka 1948.
Kauli ya Yair Lapid imekuja wakati ambapo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Eyal Zamir, alionya kuwa “jeshi la Israel liko karibu na kuporomoka.”
Israel yadai kulenga mifumo ya ulinzi wa anga na mitambo ya makombora nchini Iran
Israel imedai kulenga mifumo ya ulinzi wa anga na mitambo ya makombora katika maeneo mbalimbali nchini Iran.
Kwa mujibu wa jeshi la Israel, maeneo yaliyopo Tehran yaliyokuwa kituo cha utengenezaji wa makombora ya masafa marefu (ballistic) na silaha nyingine yalilengwa kati ya Alhamisi na usiku wa Ijumaa.
Jeshi hilo pia linadai kuwa jeshi la anga la Israel lililenga vizindua makombora na maeneo ya kuhifadhi makombora katika magharibi ya Iran.
Kwa upande mwingine, Kuwait imesema bandari yake kuu ya kibiashara imeshambuliwa na droni za “adui.”
Katika taarifa, Mamlaka ya Bandari za Kuwait ilisema kuwa Bandari ya Shuwaikh iliharibiwa, lakini hakukuwa na taarifa za majeruhi.
Marekani ilirusha mamia ya makombora ya Tomahawk dhidi ya Iran - Washington Post
Gazeti la Washington Post liliripoti siku ya Ijumaa, likinukuu vyanzo ambavyo havikutajwa jina, kwamba jeshi la Marekani limerusha zaidi ya makombora 850 ya kusafiri ya Tomahawk wakati wa vita vya wiki nne na Iran.
Ripoti hiyo ilisema kuwa utumiaji wa makombora hayo ambayo hulenga kwa usahihi shabaha zinazopigwa, ulikuwa wa kiwango cha juu, jambo ambalo lilizua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya maafisa wa Pentagon na kusababisha mijadala ya ndani kuhusu jinsi ya kuongeza idadi ya silaha hizo.
Shirika la habari la Reuters lilisema bado halijaweza kuthibitisha ripoti ya gazeti hilo, huku Wizara ya Ulinzi ya Marekani na Ikulu ya Marekani hazikujibu ombi la Reuters la kutoa maoni yao.
Je, ‘zawadi’ ya ‘meli 10 za mafuta’ zimepitia Mlango-Bahari wa Hormuz kama anavyodai Rais Trump?
Rais wa Marekani Donald Trump alidai katika kikao cha baraza la mawaziri Alhamisi kwamba Iran iliruhusu meli 10 za mafuta kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz kama ishara ya nia njema.
Rais Trump alisema kuwa Iran iliruhusu meli hizo 10 kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz kama “zawadi” kuonyesha kuwa inachukulia mazungumzo kwa uzito.
Rais huyo wa Marekani alisema kuwa “meli nane za mafuta zilizojaa mafuta zilipita (katika Mlango-Bahari wa Hormuz).”
“Niliwaza kwamba (meli hizi) zilikuwa zinabeba bendera za Pakistan. Nikasema tunazungumza na watu sahihi.”
Kisha rais wa Marekani alidai kuwa Iran iliomba radhi kwa jambo fulani ililosema hapo awali na kusema, “Tunatuma meli nyingine mbili (za mafuta) na hivyo jumla ya meli hizo imefikia 10.”
BBC Verify ilitumia data za umma za ufuatiliaji wa meli kujaribu kubaini ni meli zipi zilipita katika Mlango-Bahari huo zikiwa na vifaa vyao vya kutuma taarifa za mahali zilipo kati ya tarehe 23 na 25 Machi. Kwa mujibu wa Rais Trump, meli hizo zilipita katika kipindi hicho.
Meli tano zilizokuwa zikisafirisha mafuta kupitia Mlango-Bahari huo zilitambuliwa katika kipindi hicho, lakini hakuna iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Pakistan. Hakuna hata moja ya meli nyingine tano zilizopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz iliyoorodheshwa kama meli ya mafuta.
Wachunguzi wa ufuatiliaji wa meli huenda wasiwe na taarifa kuhusu meli zinazozima kwa muda mitambo yao ya GPS wakati zinapopita katika mlango huo.
Iran yadai kuzirudisha nyuma meli tatu za mizigo zilizojaribu kupita Mlango-Bahari wa Hormuz
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) limeeleza kuwa limezirudisha nyuma meli tatu zilizokuwa zikijaribu kupita Mlango-Bahari wa Hormuz asubuhi ya leo.
IRGC ilisema katika taarifa kwamba meli tatu za mizigo kutoka nchi tofauti zilijaribu kuelekea kwenye korido hiyo. “Zilirudishwa nyuma baada ya kuonywa na Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa “Mlango-Bahari wa Hormuz umefungwa na jaribio lolote la kupita litakabiliwa na jibu kali.”
“Chombo chochote kinachotoka au kuelekea katika bandari za washirika na wanaounga mkono Marekani na Israel hakiruhusiwi kupita kwenye korido hiyo.”
Siku mbili zilizopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, alisema katika televisheni ya taifa kuwa Iran hadi sasa imekubali maombi ya kupita kutoka kwa meli za nchi kama “China, Urusi, Pakistan, Iraq na India.” Alisema kuwa kwa mtazamo wa Iran, Mlango-Bahari wa Hormuz “haujafungwa kabisa, bali umefungwa kwa maadui pekee.”
Ikumbukwe kwamba jana, Rais wa Marekani Donald Trump alidai kuwa Iran iliruhusu meli 10 za mafuta kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz kama ishara ya nia njema.
Iran yashauri watu wa Mashariki ya Kati kuondoka maeneo yaliyo karibu na vikosi vya Marekani
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) limewaonya watu katika eneo hilo kuondoka katika maeneo ambako kuna vikosi vya Marekani.
Katika taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la Fars linalohusishwa na IRGC, walinzi hao wameishutumu Marekani na Israel kwa “kutumia maeneo ya raia na watu wasio na hatia kama ngao za binadamu.”
Taarifa hiyo pia imeishutumu Marekani kwa kuwaua raia na maafisa wa Iran.
Ikumbukwe kwamba IRGC imetoa onyo kadhaa kama hizi tangu kuanza kwa vita. Hapo awali, tarehe 14 Machi, IRGC iliwashauri wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya viwanda vya Marekani katika Mashariki ya Kati kuhama.
Hata hivyo, katika onyo hili la hivi karibuni, mamlaka za Iran hazikutaja eneo maalum na inaonekana kuwa ni onyo la jumla.
Makamanda kadhaa wakuu wa IRGC wameuawa katika vita vinavyoendelea.
Iran haijatoa takwimu zozote za vifo katika siku za hivi karibuni.
Shirika la kutetea haki za kibinadamu Human Rights Watch (HRW) lililoko Marekani limesema kuwa raia 1,492 wa Iran, wakiwemo watoto 221, wameuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, huku idadi ya wanajeshi wa Iran waliouawa ikifikia 1,167.
Uingereza yaishutumu Iran kwa kuuteka uchumi wa dunia
Mawaziri wa mambo ya nje kutoka kwa mataifa saba tajiri zaidi duniani (G7), akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper, wanakutana nchini Ufaransa. Mazungumzo yanatarajiwa kuangazia vita dhidi ya Iran.
Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza alitoa wito wa “kupatikana kwa suluhu ya haraka” ya mgogoro wa Mashariki ya Kati, akiishutumu Iran kwa “kuushikilia uchumi wa dunia mateka” kwa kuzuia Mlango-Bahari wa Hormuz.
“Ni wazi kabisa kwamba tunahitaji kuona suluhu ya haraka ya mgogoro huu ili utulivu urejee katika eneo hilo,” alisema.
Akizungumzia hatua za Iran katika Mlango-Bahari wa Hormuz, alisema:
“Iran haipaswi kuushika uchumi wa dunia mateka kwa kudhibiti tu mlango-bahari unaohusiana na njia za kimataifa za usafiri wa majini na uhuru wa usambazaji.”
Oburu Oginga aidhinishwa rasmi kuwa kinara wa Chama kikuu cha Upinzani nchini Kenya ODM
Chama kikuu cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) kimeridhia rasmi kumteua Seneta wa Siaya, Dkt. Oburu Oginga, kuwa kiongozi mkuu wa chama kufuatia kifo cha kaka yake na kiongozi wa muda mrefu wa chama, Raila Odinga, kilichotokea tarehe 15 Oktoba 2025.
Dkt. Oburu, ambaye awali alikuwa akikaimu nafasi hiyo baada ya kuteuliwa na Baraza la Kitaifa la Uongozi wa chama (NGC), aliidhinishwa rasmi kushika wadhifa huo katika Mkutano Maalum wa Wajumbe (SDC) uliofanyika Jamhuri Grounds siku ya Ijumaa.
Alipendekezwa na Mbunge wa Mumias Magharibi, Johnson Manya Naicca, na kuungwa mkono na Mbunge wa Mathare, Anthony Oluoch, baada ya hoja hiyo kuwasilishwa mbele ya wajumbe na Mkurugenzi wa Uchaguzi na Kampeni wa ODM, Junet Mohamed.
Dkt. Oburu atasaidiwa na Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Shariff Nassir, pamoja na mwenzake wa Kisii, Simba Arati, ambao pia walipendekezwa na kuungwa mkono rasmi kushika nyadhifa hizo.
Hata hivyo, Naibu Kiongozi wa chama aliyependekezwa wa tatu, Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi, hakupata mpendekezaji wala muungaji mkono, na hivyo akaondolewa katika nafasi hiyo.
Hali hii imejiri wakati Osotsi na kundi linalodaiwa kuwa la waasi ndani ya ODM linaloitwa Linda Mwananchi waliposusia mkutano wa SDC na badala yake kuandaa mkutano wao sambamba wa “Kitaifa wa Wajumbe wa Wananchi” (NDC) katika Ufungamano House.
Wakati huo huo, Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna ameshutumu polisi kwa kuwavurugia Kongamano la Wajumbe wa Kitaifa la Linda Mwananchi lililopangwa kufanyika katika jumba la ufangamano jijini Nairobi.
Sifuna alisema mrengo huo uliarifu rasmi mamlaka kuhusu mkutano huo, ambao alisisitiza ulinuiwa kuwa wa amani na sio maandamano.
Hata hivyo, wanachama waliofika katika ukumbi huo walikutana na malori yaliyokuwa yamejaa maafisa wa polisi, jambo ambalo SG alilitaja kuwa lisilo la lazima na la kutisha.
"Tulipeana ilani kwamba tutakuwa na mkutano hapa, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba malori ya polisi yamejaa hapa nje," Sifuna alisema.
Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IEA laonya hatari ya mionzi iwapo mashambulizi yataendelea Iran
Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limeonya uwezekano wa kuvuja kwa mionzi hatari iwapo mashambulizi yataendelea karibu na kituo cha nguvu za nyuklia cha Bushehr.
IAEA imetoa wito wa “kudumishwa kwa kiwango cha juu kabisa cha kujizuia” ili kuzuia uchafuzi wa mionzi nchini Iran, onyo lililotolewa kufuatia taarifa za shambulio karibu na kituo hicho kilichopo kusini mwa Iran zilizoripotiwa Jumanne.
“Kwa kuzingatia kwamba hili ni kinu hai cha nyuklia chenye kiwango kikubwa cha nyenzo za nyuklia, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi, anaonya kuwa uharibifu wowote kwa kituo hiki unaweza kusababisha kuachiliwa kwa mionzi ya nyuklia itakayoweza kuathiri maeneo mapana ndani ya Iran na hata nje ya mipaka yake,” ilisema taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa.
Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un azawadiwa bunduki
Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, amemkabidhi kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, bunduki kama zawadi, wakati walipotia saini mkataba wa urafiki mjini Pyongyang, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Viongozi hao wawili, ambao ni waungaji mkono muhimu wa vita vya Urusi nchini Ukraine, walikubaliana kuimarisha zaidi ushirikiano na kupinga shinikizo la mataifa ya Magharibi.
Lukashenko alitania akimwambia Kim kuwa amemletea bunduki ya kurusha risasi mfululizo “endapo adui atatokea,” kama inavyoonekana katika video iliyotolewa na vyombo vya habari vya Belarus.
Kwa upande wake, Kim alimkabidhi Lukashenko upanga na shoka vilivyochorwa picha yake.
“Ninakuambia kama rafiki yako, na kama mtu aliyeona sehemu nyingi za dunia: mustakabali mzuri sana unaisubiri nchi yako, kwa kuwa una watu wengi wanaofanya kazi kwa bidii na wenye nidhamu,” Lukashenko alimwambia Kim, kwa mujibu wa shirika la habari la Belarus, Belta.
Mashambulizi yafanyika usiku kucha kote Mashariki ya Kati
Israel imeendelea kushambulia
kote Iran usiku kucha, huku jeshi lake likisema asubuhi ya leo kwamba
lilishambulia maeneo ya uzalishaji wa makombora huko Tehran na kituo cha
kutengeneza vilipuzi vya baharini huko Yazd.
Mashambulizi dhidi ya Israeli
pia yaliendelea - picha zinaonyesha kile kinachoonekana kama njia za
roketi angani juu ya mji wa pwani wa Netanya
Wakati huo huo shambulizi la
Israeli lilishambulia vitongoji vya kusini mwa Beirut mapema asubuhi ya
leo, kulingana na vyombo vya habari vya Lebanon.
Bandari kuu ya kibiashara ya
Kuwait imeshambuliwa na ndege zisizo na rubani "za adui" -
mamlaka ya bandari inasema kumekuwa na "uharibifu wa vifaa"
lakini hakuna ripoti za majeruhi
Na Saudi Arabia imeripoti kuwa
ndege nyingi zisizo na rubani zimedunguliwa usiku kucha
Pia, Wall Street Journal
imeripoti kwamba Donald Trump anafikiria kutuma wanajeshi 10,000 wa
ardhini Mashariki ya Kati.
Marekani inajiandaa kwa 'shambulizi kubwa la mwisho' katika vita vya Iran
Marekani inajiandaa
kwa chaguzi za kijeshi kwa ajili ya "shambulizi kubwa la mwisho"
katika vita vya Iran, lenye kujumuisha vikosi vya ardhini na mabomu makubwa,
kulingana na ripoti ya Axios, ikinukuu maafisa wawili wa Marekani na vyanzo
viwili vyenye ufahamu wa jambo hilo.
Kulingana na
ripoti hiyo, "kuongezeka kwa wanajeshi kwa kasi" kunatarajiwa ikiwa hakutakuwa
na hatua yoyote iliyopigwa katika mazungumzo kati ya Iran na Marekani.
Trump anaweza kuchagua mapendekezo manne, ikiwa ni pamoja
na matumizi ya wanajeshi wa ardhini na uwezekano wa uvamizi wa Kisiwa cha
Kharg, sehemu muhimu ya mafuta ya Iran, kulingana na Axios.
Chanzo
kinachofahamu juhudi za mazungumzo kilisema kwamba Uturuki, Pakistan, na Misri
zinaendelea na majaribio yao ya kupanga mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Chanzo hicho
kilibainisha kuwa Iran imekataa madai ya awali ya Marekani lakini haijajiondoa
kabisa uwezekano wa kufanya mazungumzo hayo.
Meli mbili za misaada zinazoelekea Cuba hazijulikani zilipo baada ya kuondoka Mexico
Operesheni
ya utafutaji na uokoaji inaendelea katika visiwa vya Caribbean kwa meli
mbili zilizopotea zilizojaa vifaa vya kibinadamu vinavyosafiri kutoka Mexico
hadi Cuba.
Mexico
imetuma timu za wanamaji na ndege za utafutaji wa kijeshi ili kupata meli ya
Friendship and Tigger Nondo, ambayo ilikuwa na wafanyakazi wasiopungua tisa,
jeshi la wanamaji la Mexico lilisema katika taarifa.
Meli hizo
zilitarajiwa kuwasili Havana Jumanne au Jumatano, lakini hakuna mawasiliano
kutoka kwao na hakuna uthibitisho wa kuwasili kwao, jeshi la wanamaji lilisema.
Jeshi la
wanamaji la Mexico lilisema limejitolea kutumia rasilimali zote zilizopo ili
kupata meli hizo na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi.
Meli mbili
zilizopotea ziliondoka Isla Mujeres, katika jimbo la Quintana Roo la Mexico
mnamo tarehe 20 Machi.
"Manahodha
na wafanyakazi ni mabaharia wenye uzoefu, na meli zote mbili zina vifaa vya
usalama vinavyofaa na vifaa vya kuashiria," msemaji wa msafara huo alisema
katika taarifa kwa Reuters.
"Tunashirikiana
kikamilifu na mamlaka na tunasalia na imani katika uwezo wa wafanyakazi kufika
Havana salama."
Saini ya Trump kuonekana kwenye noti ya dola za Marekani
Wizara ya
Fedha ya Marekani imetangaza kuwa Donald Trump anatarajiwa kuwa rais wa kwanza
wa Marekani aliye madarakani kutia sahihi yake kwenye noti za Marekani.
Saini ya
Trump itaonekana pamoja na ile ya Waziri wa Fedha Scott Bessent, hatua ambayo
haijawahi kutokea na idara hiyo ilisema itaadhimisha kumbukumbu ya miaka 250 ya
Marekani.
"Hakuna
njia yenye nguvu zaidi ya kutambua mafanikio ya kihistoria ya nchi yetu kubwa
na Rais Donald J Trump zaidi ya noti za dola za Marekani kuwa na jina
lake," Bessent alisema.
Noti za
Marekani kwa kawaida zimekuwa na sahihi za maafisa wa wizara ya fedha.
Ni hatua ya
hivi karibuni ya utawala kuhusisha jina la Trump na programu mbalimbali za
serikali na majengo ya umma.
Noti za
kwanza za $100 (£75) zenye sahihi za Trump na Bessent zitachapishwa mwezi Juni,
na zingine zitafuata.
Noti zinazochapishwa
kwa sasa zina sahihi za Waziri wa Fedha wa Rais wa zamani wa Joe Biden, Janet
Yellen, na Mweka Hazina Lynn Malerba.
Imekuwa desturi tangu mwaka 1861 kwa sahihi ya
mweka hazina wa Marekani kuonekana kwenye noti za benki, desturi ambayo itafikia
ukomo wake chini ya mipango ya utawala wa Trump
Urusi na Ukraine zadai kuteka vijiji vilivyokumbwa na vita
Wizara ya
Ulinzi ya Urusi ilisema Alhamisi kwamba vikosi vyake vimechukua udhibiti wa
kijiji kipya cha Sheviakivka katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kharkiv la
Ukraine, katika hatua yake ya taratibu ya kuteka maeneo.
Jeshi la
Ukraine halijakiri kwamba kijiji kilichoko kwenye mpaka wa Urusi kilikuwa kimetekwa.
Kikosi cha
wanajeshi wa parachuti cha Ukraine kilisema kimeteka kijiji kilichokuwa kusini
katika eneo la Dnipropetrovsk ambacho hapo awali kilikuwa kimetawaliwa na
Urusi.
Hata hivyo, Reuters
haijaweza kuthibitisha ripoti za maeneo ya vita kwa uhuru.
Zelensky yuko Saudi Arabia huku Ukraine inawapa utaalamu wa droni
Rais wa
Ukraine Volodymyr Zelensky aliwasili Saudi Arabia siku ya Alhamisi, baada ya
kusema mapema kwamba ndege zisizo na rubani za Ukraine zinaweza kusaidia
kuboresha usalama katika eneo la Ghuba.
"Mikutano
muhimu imepangwa. Tunashukuru usaidizi wa wale walio tayari kufanya kazi nasi
ili kuhakikisha usalama, na tunawaunga mkono pia", alisema katika ujumbe
kwenye mitandao ya kijamii.
Mapema siku
ya Alhamisi, Zelensky alitoa utaalamu wa Ukraine katika teknolojia ya ndege
zisizo na rubani kama njia ya kuboresha usalama kote ulimwenguni, haswa eneo la
Ghuba.
"Hili
ni muhimu kwa sababu usalama wa nishati - na gharama ya maisha, haswa barani
Ulaya - inategemea mafuta, gesi na rasilimali zingine, na masoko thabiti ya
kimataifa," alisema katika ujumbe wa video kwa Kikosi cha Pamoja cha
Usafirishaji, muungano wa usalama ambao ulifanya mkutano wa kilele huko
Helsinki.
"Cha
msingi si tu kutengeneza silaha mpya - hasa ndege zisizo na rubani - si
teknolojia tu, bali pia uzoefu halisi katika kuzitumia, na kuziunganisha na
rada, usafiri wa anga, na mifumo mingine ya ulinzi wa anga. Tuna uzoefu
huu," alisema.
Zelensky
alisema kwamba kwa mabadilishano anatafuta msaada wa kuilinda Ukraine dhidi ya
uvamizi unaoendelea wa Urusi.
"Tungependa
mataifa ya Mashariki ya Kati pia yatupe fursa ya kujiimarisha. Yana makombora
fulani ya ulinzi wa anga ambayo hatuna ya kutosha. Hilo ndilo tungependa
kufikia makubaliano," alisema katika mahojiano na gazeti la Ufaransa la Le
Monde.
Jeshi la
Ulinzi la Israeli (IDF) linasema limekamilisha "wimbi kubwa la
mashambulizi" katika "kitovu cha Tehran", likilenga miundombinu
ya serikali.
Vyombo vya
habari vya serikali nchini Iran vilikuwa vimeripoti kwamba milipuko ilisikika
katika mji mkuu na kwamba ulinzi wa anga ulikuwa "ukikabiliana na adui".
Tutakuletea
maelezo zaidi yanapoingia.
Trump aongeza muda wa kusitisha mashambulizi kwa siku 10
Rais Donald
Trump wa Marekani amesema Iran ilimwomba asitishe mashambulizi kwa siku saba
kwenye biwanda vya nishati, lakini ameipa siku kumi, na Tehran "ikamshukuru
sana" kwa hatua hiyo.
Awali, Trump
alitangaza kwenye mtandao wa Truth Social kwamba ataongeza muda wa
kusitisha mashambulizi katika maeneo ya viwanda vya mafuta vya Iran kutoka
siku tano hadi wiki mbili.
Muda wa
kusitisha mashambulizi ulipangwa kuisha kesho, lakini hatua hii inamaanisha
kuwa usitishaji huo utaendelea kutekelezwa hadi Aprili 6.
Akizungumza
kwa njia ya simu na Fox News hivi karibuni, Trump alisema Marekani iko kwenye
mazungumzo na Iran ambayo yanaendelea "vizuri".
"Waliniambia,
kwa uzuri sana, kupitia watu wangu: 'Tunaweza kuwa na muda zaidi?'," rais
wa Marekani aliwaambia watangazaji wa kipindi cha Fox's The Five.
"Waliomba
[siku] saba. Nami nikasema, 'Nitawapa kumi', kwa sababu walinipa meli. Unajua,
tulizungumzia kuhusu meli nane. 'Zawadi' niliyozungumzia ile siku
nyingine."
Katika
mkutano wa baraza la mawaziri la Ikulu mapema leo, Trump alisema Iran
iliruhusu meli za mafuta kupita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz kama
"zawadi" kwake wakati wa mazungumzo.
Hata hivyo, Iran
imekanusha kwamba mazungumzo ya kukomesha vita yanaendelea.
Facts Only
The U.S. military conducted airstrikes in Syria targeting facilities used by Iran-backed militia groups
Iran announced it would no longer adhere to some limits set by the nuclear agreement
President Trump has expressed his intention to negotiate with Iran over the nuclear deal
Executive Summary
Full Take
The escalation in tensions between the U.S. and Iran comes after months of increased rhetoric and actions from both sides. This latest development appears to be a response to the U.S.'s withdrawal from the Iran nuclear deal and subsequent sanctions, as well as Iran's continued support for militia groups in Syria and Iraq.
The U.S.'s decision to strike Syria raises questions about the limits of American military intervention in the region, particularly given Trump's previous criticisms of U.S. involvement in Syria. Meanwhile, Iran's announcement that it would no longer abide by certain limitations set by the nuclear deal suggests a hardening of its stance and a potential escalation in the standoff between the two nations.
It remains unclear what the long-term implications of these actions will be, both for the region and for global efforts to prevent the proliferation of nuclear weapons. The situation serves as a reminder of the complex web of relationships and geopolitical interests at play in the Middle East, and the potential for sudden, unpredictable events to further complicate an already volatile region.
